
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya
Pia ameiagiza Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kufuatilia na kuhakikisha kuwa taarifa na malalamiko yanayoletwa na watumiaji wa barabara yanafanyiwa kazi kwa wakati na Wakala wa Barabara.
Naibu Waziri Kasekenya ametoa maagizo hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwenye miundombinu ya barabara, iliyoambatana na uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali barabara, iliyofanyika jijini Mwanza.
Ambapo ameeleza kuwa ameziagiza TANROADS na TARURA kuzifanyia kazi kwa wakati taarifa zinazoletwa kwao na watumiaji wa barabara kwa lengo la utekelezaji.
"Upatikanaji wa taarifa za hali ya barabara kwa wakati, ni moja ya njia muhimu za kutunza miundombinu ya barabara, naipongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kubuni mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa na wananchi na watumia barabara kufuatilia na kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya hali ya barabara katika maeneo yao,"ameeleza Kasekenya.
Pia ameendelea kwa kuziagiza TANROADS na TARURA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye madaraja na makalavati ili kuepuka kutokea kwa majanga makubwa kama lile la Kiyegeya.